Tumia sana ujuzi na uzoefu wako kujaza pengo katika soko.

Submitted by admin on
Display title
Tumia sana ujuzi na uzoefu wako kujaza pengo katika soko.
Bio
Image
Display name
Susan Mashibe - Tanzania, United Republic of
Susan Mashibe ni rubani wa ndege za kibiashara aliyepewa kibali na Shirikisho la Anga la Marekani (FAA) na pia ni mhandisi wa kukarabati ndege, mwanamke wa kwanza Mtanzania aliyefuzu katika nyanja hizo mbili. Baada ya kufuzu kutoka Marekani, alienda nyumbani Tanzania kuanzisha biashara katika sekta changa ya Biashara ya Usafiri wa Anga ya Afrika. Sasa hivi akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa biashara yake mwenyewe iliyonawiri ya VIA Aviation, anaelezea changamoto zake, na matumaini yake siku za usoni.


Story

Nilizaliwa na kukulia Tanzania. Ndoto yangu ya urubani ilianzia katika uwanja mdogo wa ndege huko Kigoma, katika fuo za Ziwa Tanganyika. Wakati nikiwa na miaka minne, wazazi wangu pamoja na ndugu zangu wadogo walipaa kwa ndege hadi Dar es Salaam, wakaniacha nikae na nyanyangu. Wakati ndege iliyowabeba ilipaa angani, sikulia. Ila, nilitamani kwamba ningeendesha ndege hiyo mimi mwenyewe, ili wazazi wangu wasiniache nyuma tena.

Leo, ninaendesha biashara yangu mwenyewe katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Kutokea mwaka wa 2002, VIA Aviation, ambayo mwanzo iliitwa Jet Centre, inatoa huduma ya eneo maalum kama vile kutia ndege mafuta, huduma ya chakula, usafi na itifaki huko Tanzania. VIA lilikuwa shirika la kwanza kutoa huduma kama hizo Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla. 

Imekuwa safari ndefu hadi kufika hapa. Dada yangu alikuwa akihudhuria chuo huko Marekani, kwa hivyo, nilipokamilisha shule Tanzania, nilisafiri hadi Michigan Marekani kusomea urubani.  Nilikuwa na miaka 19 nilipofanya somo langu la kwanza la kuendesha ndege angani. Mwanzoni, kutokana na udhaifu wangu wa kuwasiliana katika Kingereza, ilikuwa na maana kuwa nisingeweza kuwasiliana na mnara wa kuongozea ndege, kwa hivyo, sikuweza kuendesha ndege peke yangu. Mwelekezi wangu alinishauru niimarishe Kiingereza changu cha kuzungumza kisha nijifunze tena. Wakati nilikuwa ninasoma Kiingereza, nilijisajili kwenye mradi wa chuo wa kukarabati ndege kusomea mifumo ya ndege. Nilipokamilisha, nilikuwa nimetimiza mahitaji yote ya kusajiliwa kuwa fundi wa mwili wa ndege na mfumo wa umeme na Shirikisho la Anga la Marekani (FAA).  

Hivyo ndivyo nilikuwa mhandisi wa kukarabati ndege bila kukusudia, jambo ambalo liliniwezesha kufanya kazi huku nikiendelea kupata elimu yangu ya urubani. Ili kuendelea kuwa na viza (visa) ya kuniruhusu kuishi Marekani kama mwanafunzi, nililazimika kuongeza masomo mengine zaidi. Kwa hivyo, nilijisajili kusomea Shahada ya Usimamazi wa Safari za Angani (Aviation Management Degree).

Ndoto yangu ilikuwa kuwa rubani wa kitaalamu anayelifanyia shirika moja maarufu la ndege za abiria la Marekani. Hata hivyo, nilikamilisha mafunzo yangu ya urubani wa ndege za abiria mnamo Septemba 11, 2001. Mashambulizi mabaya ya kigaidi yaliyofanyika wakati huo yalitikisa sekta ya uchukuzi wa angani, na ajira kwa marubani ikawa ngumu sana kupatikana. Huku muda wa viza yangu ya masomo ukikaribia kumalizika, ilinibidi nitafute mpango mwingine mbadala. Hapo ndipo nilipoamua kurudi Tanzania na kuanzisha shirika langu mwenyewe.        

VIA Aviation hutoa huduma muhimu ambazo husaidia biashara nyingine kukua katika bara nzima. Wakati chumi za nchi nyingi barani zinapopitia kipindi cha ukuaji wa haraka, kukosekana kwa barabara nzuri, na miundomsingi ya reli kumekuwa changamoto kubwa. Ni vigumu sana kusafiri kwa barabara baina ya miji mingi mikuu – hizi zikiwa pamoja na barabara zinazounganisha miji inayopatikana kwenye taifa moja. Licha ya haya yote, ni asilimia 20 pekee ya safari za angani barani ni za Kiafrika. Hii ina maana kwamba wasafiri mara nyingi watasafiri hadi Ulaya au Mashariki ya Kati ili kuunganisha safari ya taifa jingine la Afrika. Hii ni ghali na hupoteza muda na, wakati ambapo chumi za Afrika zinaimarika, haikubaliki kwa wanaoongoza biashara kwani wengi wao sasa wanakodisha ndege za kibinafsi. Hapo ndipo biashara yangu inaingilia – kwa kutoa huduma za kitaalamu, ambazo ni huduma za hali ya juu kwa ndege za kibinafi. VIA Aviation hujaza pengo lililoko katika ndege za kibinafsi. VIA Aviation hujaza mahitaji yaliyoko sokoni. Sasa hivi tuna mapato zaidi ya Dola milioni 2, na nina mipango wa kupanua ili kufikia zaidi ya mataifa 20 Afika nzima.    

Uamuzi mmoja muhimu niliofanya ulikuwa kwamba VIA Aviation ingekuwa kampuni ya kwanza ya yenye upekee wa aina yake katika Afrika Mashariki wa kukukubali kadi maalumu za mikopo kama vile Avcard, Colt, MultiService, na UVair pamoja na Viza na MasterCard. Asilimia 90 ya shughuli za VIA ni za kielektroniki, jambo linalosaidia kuondoa ufisadi na pia kuondoa hali inayowalazimu wasafiri kubeba pesa nyingi kulipia mafuta.

Kama mwanamke katika biashara, na katika uwanja ambao umemilikiwa na wamaume, nimekumbana na changamoto nyingi; kutoka kwa maafisa wanaume wa uwanja ndege ambao wamenizuia nisiingie kwenye ndege ninayohudumia, hadi kwa wateja wangu ambao lazima nithibitishe kwamba ni mimi. Pia nimekabiliana na maafisa fisadi ambao watasisitiza wapewe hongo kwa kazi ndogo tu. Ninapokabiliwa na changamoto hizi, mtazamo wangu daima umekuwa mmoja: kuwa jasiri na mwaminifu. Nina imani na biashara yangu, na faida ambazo tunaleta kwa wateja na kwa serikali ya Tanzania.

Kama mjasiriamali mwanamke aliyefanikiwa, ninatambua kwamba nina majukumu ya kuwapa msaada wale wanaofuata nyayo zangu, na kuisaidia jamii.

Maswali kwa msomaji:

1. Je, stadi zako za lugha ziko vipi? Je, wahitaji kujifundisha lugha mpya au upige msasa lugha yako ambayo tayari waijua ili kujiimarisha wewe mwenyewe pamoja na biashara yako?

2. Je, umetambua mapengo sokoni, ambayo yanaweza kujazwa kutumia maarifa yako na tajriba?

3. Je, huduma sawa zaweza kutumiwa katika biashara yako ili kukusaidia kupata wateja zaidi kwenye biashara yako? 

Lessons

1. Uvumbuzi wa bidhaa: Kuwa mbunifu na utalii soko (na mapengo sokoni) ili kutambua namna bidhaa zako na huduma zinavyoweza kuongeza thamani na kujaza pengo muhimu.

2. Upanuzi wa soko: Tambua wateja wapya na fikiria kuhusu huduma za ziada ambazo zinaweza kukusaidia kukuza soko la bidhaa zako.

3. Maadili ya biashara: Kukua jasiri na mwaminifu ni sifa ambazo zitaleta manufaa katika muda mrefu ujao.