Panua kampuni yako kwa kutoa mafunzo na kuwawezesha wengine kutoa huduma za biashara yako.

Submitted by admin on
Display title
Panua kampuni yako kwa kutoa mafunzo na kuwawezesha wengine kutoa huduma za biashara yako.
Bio
Image
Display name
Lina Khalifeh – Jordan
Lina Khalifeh ni mwanzilishi wa SheFighter "Kituo cha kwanza cha kutoa mafunzo ya kujikinga mwenyewe kwa wanawake huko Mashariki ya Kati". Ana Mkanda Mweusi (Black belt) katika mchezo wa Taekwondo 3DAN, kupigana mateke (KickBoxing) na anafurahishwa sana na kuwawezesha wanawake kwa mafunzo ya Sanaa ya maungo ya Kujikinga (Martial Arts).


Story

Miaka minne iliyopita, niliwazia kuhusu kuwapa wanawake mafunzo ya namna ya kujikinga wenyewe. Kama mtaalamu wa mkanda mweusi wa Taekwondo, nilikuwa nimehitimu, lakini nilichelea. Wanawake wengi hawapendi kujiingiza katika mafunzo ya sanaa hii ya kujikinga iliyomilikiwa na wanaume. Wazo la kuanzisha biashara Jordan, ambayo ni nchi yangu, lilikuwa hata gumu zaidi kwa sababu ya utamaduni wenye taasubi ya kiume, huku wanawake haswa kutoka mashambani kwa kawaida wakiwa hawana uhuru wa kujieleza.

Sikuwa peke yangu ambaye sikuwa na hakika. Marafiki, familia na hata wageni walinitahadharisha dhidi ya kutojihusisha na biashara ambayo inakiuka matarajio ya jamii namna wanawake wanafaa kuishi. Hata hivyo, nilijaribu. Niliweka tangazo la biashara yangu ya SheFighter kwenye karatasi dogo katika sehemu ya chini ya nyumba yangu. Kinyume na matajio yangu, nilianza kupokea simu.

Wateja wangu wa kwanza kabisa walikuwa wanawake wawili wenye umri wa makamo waliotaka kujifunza namna ya kujikinga ili wawe na ujasiri na wawe na miili yenye nguvu. Nia yao na kufurahi kwao vilinipa msukumo niliohitaji wa kujitolea kuifanikisha biashara yangu. Wanawake hawa wawili walifurahia mafunzo yao ya kwanza, na wakawa wanarudi na rafiki zao kila mara. Nilianza kupokea simu zaidi na wateja wengi zaidi.

Ndipo nilipotambua kuwa wanawake wanahitaji, na wanataka, maarifa ya kujikinga zaidi ya mwanaume yeyote huko Jordan.

Kwangu mie, kuwa kiongozi ina maana kuwa na ujasiri wa kutosha kutambua nguvu zako za ndani. Kujikinga kunawapa wanawake nguvu. Kunaongeza nguvu zao za mwili, zaidi ya yote, kunainua kujiamini kwao. Nimewaona wanawake na wasichana ambao walijihisi hawana nguvu wakibadilika na kuwa viongozi jasiri.

Katika mwaka wa 2012, baada ya kutoa mafunzo nikitumia sehemu ya chini ya nyumba yangu (basement), nilifungua kituo cha SheFighter kwa wanawake wa Mashariki ya Kati.

Mwaka wa 2013, kituo cha SheFighter kilikuwa na mafanikio zaidi ya vituo vyote vya mazoezi Jordan. Kwa kutoa maelekezo bora na mazingira ambayo yanawafanya wanawake kuhisi vizuri, bidhaa yetu na sifa zetu zimeenea sana kwa njia ya mdomo.

Tuko mbioni kufikia lengo letu la kuwawezesha wanawake milioni tatu Mashariki ya Kati kufikia mwaka wa 2020. Mpango wetu wa mafunzo kwa wakufunzi unafawafundisha wanafunzi wa SheFighter kugawa ujuzi wao kwa wanawake wanaoishi mashambani. Kwa maoni yangu, wanawake hawa wa mashambani ndio wanahitaji programu hii yetu zaidi.

Nimekuwa kiongozi kwa kufuata ndoto yangu ya kutoa mafunzo ya kujikinga na kuwawezesha wanawake. Katika kituo cha SheFighter, tunawasaidia wanawake wengine wawe viongozi kwa kuwahimiza wawe kile wanataka kuwa.

Kila mara ninaona wanawake wakijidunisha. Wengi wao hawaoni nguvu waliyo nayo ndani yao ya kuwa viongozi wa ajabu. Katika nyakati hizi, huwa ninaanza kwa kutaja nukuu ninayoipenda, “Zungumza bila kuogopa, hata sauti yako ikitetemeka.”

Tulianzisha mradi wa kwanza nchini Armenia mwaka wa 2014. Utamaduni wa huko ni tofauti na ule wa Jordan, ila tunatia juhudi kujenga mazingira ya SheFighter Armenia ambayo yanaingiliana na jamii na utamaduni wao.

Niliamua kukinga chapa yetu ya SheFighter katika mwaka wetu wa kwanza wa biashara, kwani nilijua kwamba kituo hiki kingeshindana na vituo vingine vingi vyenye kutoa mafunzo ya kujikinga. Nilifanya hivyo hivyo kwa kukisajili na kukikinga kituo hiki chini ya Sheria za milki dhihini za Jordan (Jordan’s intellectual property laws). Bado tunashughulikia uwezekano wa kukisajili kituo hiki kimataifa.  

SheFighter huendesha shughuli zake za kila siku kutokana na ada ya uanachama na usajili; hatujawa na msaada wowote wa kifedha kutoka katika shirika lolote Jordan au kokote.

Mwezi wa Oktoba mwaka wa 2014, nilichukua nafasi ya kwanza katika tuzo ya Empretec Women in Business Global. Kupokea tuzo hii katika Umoja wa Mataifa huko Geneva kulinipa mimi na kikosi changu msukumo mkuu wa kuendelea, na kufungua macho yangu kwa uwezekano wa kupanua SheFighter, na kuufikia ulimwengu mzima.

Maswali kwa msomaji:

1. Maono yako ni yapi? Je, unaweza kugeuza maono hayo yako kuwa msukumo na nguvu unayohitaji kufanya biashara yako ifanikiwe?

2. Je, umezingatia namna mtindo wa biashara unaotumia unaweza ukasaidia biashara yako kukua? Utatumia mtindo upi kupanua upeo wa bidhaa zako na huduma? Je, kuitafutia kibali cha kufanyia biashara je?

3. Je, unafuatalia wanayofanya washindani wako? Je, umekinga chapa ya bidhaa yako?

Lessons

1. Usimamizi wa wafanyakazi: Kukuza kampuni kunahusisha kusimamia watu na kujenga uwezo wao kupitia mafunzo na ushauri. Mafunzo ya wakufunzi ni wazo ambalo linaweza kusaidia kukuza watendakazi kwa maarifa na stadi zinazohitajika kutoa huduma zaidi ya uwezo wako wa kibinafsi.  

2. Kudhibiti uvumbuzi na hatari: Uvumbuzi ni hatari ila unaweza kuleta mafanikio makubwa. Kuwa na ujasiri. Chunguza shauku yoyote na pima madhara ya hatari iliyopo. Kama madhara yatakuwa makubwa, weka mpango wa kudhibiti hatari na kuigeuza kuwa mafanikio.

3. Maoni ya wateja: Tumia maoni ya wateja kuwa na kubaki mwenye ushindani mkubwa. Waamini wateja wako: wanaweza wakakueleza kama wazo lako la biashara, bidhaa au huduma ni nzuri na zitadumu, na sehemu unayohitaji kuboresha.